Okwi ndiye mchezaji bora wa kwanza ligi kuu msimu huu
Mshambuliaji
wa Simba ya Dar es Salaam, Emmanuel Okwi amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa
Agosti wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2017/2018.
Okwi alitwaa
tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili katika uchambuzi uliofanywa Dar es
Salaam jana (Jumatano) na Kamati ya Tuzo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), kutokana na mapendekezo kutoka kwa makocha wa viwanja
mbalimbali ambavyo ligi hiyo inachezwa. Wachezaji wote hao timu zao zilishinda.
Walioshindana
na Okwi katika hatua hiyo ya mwisho ni kiungo wa Mtibwa Sugar, Mohammed Issa
ambaye alisaidia timu yake kupata pointi tatu kwa ushindi wa bao 1-0 katika
mchezo dhidi ya Stand United uliofanyika Uwanja wa Manungu, Turiani, ambapo
alikuwa nyota wa mchezo huo. Mwingine aliyeshindana na Okwi ni Boniface Maganga
wa Mbao FC.
Maganga
alitoa mchango mkubwa katika ushindi wa ugenini wa bao 1-0, ambao timu yake
iliupata dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba ikiwa ni
pamoja na kufunga bao hilo.
Ushindi wa
Okwi unatokana na kutoa mchango mkubwa katika mchezo wa Simba dhidi ya Ruvu
Shooting uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na timu yake kuibuka na
ushindi wa mabao 7-0, huku Okwi akifunga mabao manne.
Pia Okwi
amekuwa mchezaji wa kwanza msimu huu kufunga hattrick (mabao matatu
katika mchezo mmoja) katika Ligi Kuu ya Vodacom inayoshirikisha timu
16, ambapo hat trick hiyo alifunga ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Mwezi huo ulikuwa
na raundi moja tu iliyochezwa Agosti 26 na 27 mwaka huu ambapo kila timu
ilicheza mechi moja.
No comments: