Buswita Atolewa Kifungoni kwa Sharti Moja tu
KAMATI ya Katiba, Sheria na Hadhi za wachezaji chini ya mwenyekiti wake, Elias Mwanjala, imetangaza kuafiki makubaliano ya Simba na Yanga kuhusu mchezaji Pius Buswita ambaye alifungiwa kwa kusaini mikataba ya timu hizo mbili ndani ya msimu mmoja.
Buswita ambaye msimu uliopita alikuwa akiicheza Mbao FC, alisaini Simba mkataba wa awali na kuchukua kiasi cha shilingi milioni 10 za Tanzania, kisha baadaye akasaini Yanga, kitendo ambacho ni kinyume na kanuni za usajili ambayo hairuhusu mchezaji mmoja kusaini timu mbili ndani ya msimu mmoja.
Kutokana na kosa hilo, Buswita akafungiwa kutocheza soka kwa kipindi cha mwaka mmoja, lakini baada ya Simba na Yanga kukubaliana namna ya kumalizana, sasa mchezaji huyo anaweza kuichezea Yanga msimu huu kwa sharti moja tu, la kuirudishia Simba shilingi milioni 10 alizochukua.
Mwanjala amesema, mchezaji huyo ataanza kucheza pindi atakapolipa pesa hizo, lakini kama hatolipa, ataendelea kukaa nje hata kama ni kipindi chote cha mkataba wake.
No comments: