Ligi Kuu Bara msimu wa 2017/18 kulindima kesho, TFF yatoa onyo kali
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL),
msimu wa 2017/18 inaanza rasmi kesho Jumamosi Agosti 26, 2017 kwa michezo saba
itayochezwa katika viwanja tofauti nchini.
Ni msimu mpya utakaotoa timu bingwa mpya
itakayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika inayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa
Miguu Afrika (CAF), msimu wa 2019.
Itakumbukwa, msimu wa CAF wa 2018, timu itakayoiwakilisha nchi
ni Young Africans SC ambayo ni Bingwa wa VPL msimu 2016/17 wakati michuano ya
Kombe la Shirikisho, Tanzania itawakilishwa na Simba SC.
TFF tunazitakia kila la kheri timu zote zinazoshiriki ligi hii,
tukiamini kwamba uadilifu utaongoza mbele ya taratibu, kanuni na sheria
zinazosimamia mpira wa miguu hapa nchini na kwingineko.
Kwa mechi za kesho Jumamosi, Simba inatarajiwa kuwa mwenyeji wa
Ruvu Shooting katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam wakati
Mbao watakuwa wageni wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Mchezo mwingine utakuwa ni kati ya Majimaji ya Songea itakayosafiri
hadi Mbeya kucheza na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini humo huku
Njombe Mji ikiialika Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Sabasaba huko
Makambako.
Kadhalika Uwanja wa Manungu ulioko Turiani, Mtibwa mkoani
Morogoro, Mtibwa Sugar itaikaribisha Stand United ya Shinyanga kwenye mchezo
mwingine wa VPL ilihali Azam atakuwa mgeni wa Ndanda FC kwenye Uwanja wa
Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Mwadui watakuwa wenyeji wa Singida United ya Singida kwenye
Uwanja wa Mwadui huko Shinyanga na Jumapili kutakuwa na Mchezo mmoja
utakaokutanisha Young Africans na Lipuli kwenye Uwanja wa Uhuru jijini.
No comments: