Header Ads

Headline
recent

NYOTA 11 BORA WATAKAOIKOSA KOMBE LA DUNIA MWAKANI

JANA Jumanne ilipigwa michezo ya mwisho ya kufuzu kwa Kombe la Dunia ambayo itafanyika mwakani nchini Urusi.

Katika michezo hiyo, ilishuhudiwa maajabu ambayo timu zilizokuwa zikipewa nafasi ya kufuzu lakini zikaikosa nafasi hiyo. Mbali na hizo, zipo zingine ambazo zimeshindwa kufuzu moja kwa moja ambapo kwa sasa zinasubiri kucheza mechi za 'play off'.

Kutokana na hali hiyo, wafahamu nyota ambao wanatesa kwenye soka la Ulaya lakini michuano hiyo wataishuhudia kupitia runinga. Nyota hao wamewekwa kwenye kikosi kimoja ambacho kinatumia mfumo wa 3-4-3.

KIKOSI
MLINDA MLANGO: Jan Oblak, Slovenia na Atletico Madrid

NI mlinda mlango wa Atletico Madrid na amekuwa na kiwango kizuri hali ambayo imemfanya kocha wake, Diego Simeone kumpa nafasi ya kwanza klabuni kwake.

Oblak (24) alikuwa ana ndoto za kushiriki Kombe la Dunia, lakini kwa bahati mbaya akaikosa hiyo nafasi. Katika maisha yake ya soka bado hajashiriki michuano hiyo.

BEKI WA KULIA: Antonio Valencia, Ecuador na Manchester United

AMEKUWA na kiwango kizuri na ni msaada mkubwa katika klabu yake ya Manchester United. Timu yake ya taifa ya Ecuador, haijafuzu Kombe la Dunia kwani imemaliza nafasi ya nane kati ya timu kumi kutoka Amerika Kusini.


BEKI WA KUSHOTO: David Alaba, Austria na Bayern Munich

Alaba aliukosa mchezo wa mwisho wa wa kufuzu Kombe la Dunia ambapo timu yake ya Austria ilikubali kichapo cha mabao 3-2.


BEKI WA KATI: Virgil van Dijk, Uholanzi na Southampton

UNAWEZA kusema ni kipindi kibaya zaidi kwa beki huyu kwani miezi michache iliyopita alifeli kuihama Southampton na kutua Liverpool. Naye hatokuwepo katika michuano hiyo kutokana na timu yake ya taifa ya Uholanzi kumaliza nafasi ya tatu kwenye Kundi A nyuma ya Ufaransa na Sweden.


KIUNGO: Arjen Robben, Uholanzi na Bayern Munich

LICHA ya kuifungia timu yake ya Uholanzi mabao 2-0 dhidi ya Sweden, lakini ushindi huo haukuifanya timu hiyo kufuzu Kombe la Dunia baada ya kumaliza nafasi ya tatu.


KIUNGO: Naby Keita, Guinea na RB Leipzig

KIUNGO huyu wa Guinea, timu yake imeshindwa kufuzu Kombe la Dunia kutoka Ukanda wa Afrika. Kundi lake ilikuwa na Libya, DR Congo na Tunisia.

KIUNGO: Arturo Vidal, Chile na Bayern Munich

Chile imeshindwa kufuzu Kombe la Dunia kutokea Ukanda wa Amerika Kusini. Katika mchezo wa mwisho ambao Vidal hakucheza kutokana na kutumikia adhabu, Chile ilikubali kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Brazil na kumaliza nafasi ya sita.


KIUNGO: Christian Pulisic, Marekani na Borussia Dortmund

AKIWA na miaka 19, Pulisic amekuwa mchezaji muhimu katika timu yake ya taifa ya Marekani na Borussia Dortmund. Baada ya USA kufungwa mabao 2-1 na Trinidad and Tobago, jana Jumanne, sasa ni dhahiri Pulisic ataishuhudia michuano hiyo kupitia runinga.


MSHAMBULIAJI: Gareth Bale, Wales na Real Madrid

Wales ilikuwa na kiwango bora kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Ulaya ambapo ilifika hatua ya nusu fainali kabla ya kufungwa na mabingwa wa michuano hiyo, Ureno. Bale ambaye alikosa michezo miwili ya mwisho kutokana na kuwa majeruhi, katika mchezo wa mwisho alishindwa kuisaidia timu yake na kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Ireland.


MSHAMBULIAJI: Pierre-Emerick Aubameyang, Gabon na Borussia Dortmund

Aubameyang amekuwa akifunga sana akiwa na Borussia Dortmund, lakini ameshindwa kuibeba Gabon katika kufuzu Kombe la Dunia.


MSHAMBULIAJI: Alexis Sanchez, Chile na Arsenal
KAMA ilivyokuwa kwa Van Dijk, Sanchez naye alikwama siku ya mwisho kuihama Arsenal kwenda Manchester City, akabaki Arsenal na kukosa kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, na sasa ameshindwa tena kufuzu Kombe la Dunia akiwa na Chile.

WACHEZAJI WA AKIBA:

Jasper Cillessen (Uholanzi na Barcelona), Daley Blind (Uholanzi na Manchester United), Miralem Pjanic (Bosnia and Herzegovina na Juventus), Marek Hamsik (Slovakia na Napoli), Henrikh Mkhitaryan (Armenia na Manchester United), Aaron Ramsey (Wales na Arsenal), Gary Medel (Chile na Besiktas).

No comments:

Powered by Blogger.